Trump azungumzia hali katika mpaka wa Mexico na Marekani
Rais wa Marekani, Donald Trump amesema hali iliyopo katika mpaka wa Marekani na Mexico inazidi kuwa mbaya na imegeuka kuwa mzozo. Kauli hiyo ameitoa jana usiku katika Ikulu ya Marekani wakati akilihutubia taifa. Trump amesisitiza kuwa hatua ya kushindwa kuwadhibiti wahamiaji haramu, inawaumiza mamilioni ya wananchi wa Marekani. Amesema mzozo wa kibinaadamu na kiusalama unaongezeka katika mpaka huo uliopo kusini mwa Marekani. Rais Trump amesema kila siku maafisa wa forodha na walinzi wa mpakani wanakabiliana na maelfu ya wahamiaji haramu wanaojaribu kuingia nchini Marekani. Kiongozi huyo amerudia wito wake wa kujengwa ukuta katika mpaka huo, akisema ni muhimu kwa usalama kwenye mpaka huo. Spika wa Baraza la Wawakilishi, Nancy Pelosi amemuonya Trump aache kuishikilia serikali ya Marekani mateka kwa kutengeneza mzozo kwenye mpaka huo na amemtaka azifungue baadhi ya shughuli za serikali ambazo zimefungwa.
No comments: