Rais Erdogan amekataa kukutana na Bolton
Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani John Bolton aliyejaribu kufanya mashauriano kuhusu usalama wa washirika wa kikurdi kaskazini mashariki mwa Syria inaonekana amepuuzwa na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.
Rais Erdogan amesema leo (08.01.2019) Uturuki haiwezi kukubali kauli ya hivi karibuni ya John Bolton, mshauri wa usalama wa rais wa Marekani Donald Trump, kwamba serikali ya mjini Ankara lazima ihakikishe usalama wa Wakurdi, ambao ni washirika wa Marekani. Akizungumza na wanachama wa chama cha AP bungeni, Erdogan amesema Bolton ameteleza.
"Kuhusu suala hili Bolton amefanya kosa kubwa, na anayefikiria namna hii pia amefanya kosa. Hatuwezi kubadili msimamo wetu kuhusu suala hili. Wale ambao ni sehemu ya ukanda wa ugaidi nchini Syria watapata funzo wanalostahiki. Hakuna tofauti hata moja kati ya PKK, YPG, PYD na Daesh."
Rais Erdogan aidha amesema Uturuki kwa kiwango kikubwa imekamilisha maandalizi ya kufanya harakati ya kijeshi dhidi ya kundi linalojiita dola la kiislamu IS nchini Syria. Uturuki inasisitiza hatua zake za kijeshi zinawalenga wapiganaji wa kikurdi nchini Syria, YPG, inaowachukulia kama magaidi, na wala sio raia wa kikurdi.
Bolton amekutana kwa kipindi cha takriban masaa mawili na mwenzake wa Uturuki, Ibrahim Kalin, na maafisa wengine wa ngazi ya juu lakini hakupata hakikisho lolote kuhusu usalama wa wakurdi, sharti muhimu katika mpango wa rais Trump kuwaondoa wanajeshi wa Marekani kaskazini mashariki mwa Syria.
Bolton pia amewasilisha ujumbe wa rais Trump akisisitiza Uturuki iache kuwashambulia wapiganaji wa vikosi vya kikurdi walioshirikiana na wanajeshi wa Marekani kupambana na wanamgambo wa kundi la dola la kiislamu, jambo ambalo Uturuki haiko tayari kulikubali.
Erdogan akataa kukutana na Bolton
Mshauri huyo anatarajiwa kuondoka Uturuki bila kukutana na rais Erdogan, mkutano ambao maafisa wa Marekani walisema Jumamosi iliyopita kwamba ulitarajiwa.
Msemaji wa Bolton, Garetth Maquis amesema maafisa wa Marekani wamefahamishwa kuwa Erdogan hangeweza kukutana naye kutokana na kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa na hotuba aliyotakiwa kuitoa bungeni hivi leo.
Wakati haya yakiarifiwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani, Mike Pompeo, amewasili mjini Amman nchini Jordan, kituo chake cha kwanza cha ziara ya siku nane Mashariki ya Kati inayonuia kuonyesha mshikamano na eneo hilo baada ya rais Trump kutangaza kuwaondoa wanajeshi wa Marekani kutoka Syria.
Pompeo anatarajiwa kutoa hotuba kuhusu sera ya Mashariki ya Kati nchini Misri, ambako rais wa nchi hiyo, Abdel Fatah al Sisi amekuwa mshirika muhimu wa Trump. Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani atazuru pia Manama, Bahrain, Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, Doha, Qatar, Riyadh Saudi Arabia, Muscat Oman, Kuwait na pengine Baghdad, Iraq.
Mwandishi: Josephat Charo/afpe/ape
Mhariri: Caro Robi
No comments: