Mgombea wa upinzani Martin Fayulu ameonya tume ya uchaguzi kutoficha ukweli
Mgombea wa urais wa upinzani nchini Congo DRC Martin Fayulu amewaonya maafisa wa uchaguzi dhidi ya ''kuficha ukweli'' huku hali ya taharuki ikiendelea kutanda baada ya matokeo ya uchaguzi kucheleweshwa.
Bwana Fayulu amesema "watu wa Congo tayari wanajua" matokeo ya uchaguzi uliyofanyika Desemba 30 kuahirishwa kwa wiki moja.
Matokeo ya awali ya uchaguzi huo yalitarajiwa kutangazwa siku ya Jumapili ya Januari 6 lakini yakaahirishwa.
- Maandamano yazidi kurindima Sudan
- CAG anaweza kukamatwa kwa amri ya Spika Ndugai Tanzania?
- Je kuna mapinduzi machache Afrika?
Uchaguzi huo ulikuwa wa kumtafuta mrithi wa rais Joseph Kabila, ambaye anaachia madaraka baada ya kuongoza nchi hiyo ya maziwa makuu kwa miaka 18.
Kabila ameahidi kwamba uchaguzi huo ambao ulikuwa umepangwa ufanyike miaka miwili uliyopita utakuwa wa kwanza wa kupokezana madaraka kwa njia ya kidemokrasia nchini DR Congo tangu taifa hilo lilipojinyakulia uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.
Mrithi wake anayempendelea ambaye pia ni waziri wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Shadary,anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wagombea wa upinzani Martin Fayulu,tajiri mkubwa wa mafuta na Felix Tshisekedi, mwana wa kiume wa kigogo wa upinzani.
Siku wa Jumanne, Bwana Fayulu alisema Tume ya uchaguzi (Ceni) lazima "itangaze matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais hivi karibuni," akiongeza kuwa: "Matokeo ya uchaguzi kamwe haina mjadala."
Awali mkuu wa tume ya uchaguzi, Corneille Nangaa, alisema kuwa kura kutoka baadhi ya vituo vya kupigia kura bado hazijahesabiwa.
Bwana Nangaa, ambaye hajasema nilini matokeo ya awali yatatangazwa ametoa wito kwa watu kuwa na subira licha ya hali ya wasiwasi inayoendelea kushuhudiwa nchini kutokana na kucheleshwa kwa matokeo ya uchaguzi.
Huku hayo yakijiri kanisa katoliki ambalo lilitoa jumla ya waangalizi 40,000 limesema kuwa linajua ni nani aliyeshinda uchaguzi.
Tamko hilo limekosolewa vikali na maafisa wa serikali ya bwana Kabila.
Siku moja baada ya uchaguzi huduma ya mawasiliano ya intaneti yalifungwa katika miji muhimu ya taifa la DR Congo katika hatua ambayo serikali ilesema ni ya kudhibiti kusambazwa kwa matokeo ya uchaguzi amabyo sio rasmi
Mwezi uliyopita rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa wanajeshi 80 wa nchi hiyo wamepelekwa katika taifa jirani la Gabon ili kuwapa ulinzi raia wake nchini DRC endapo ghasia zitatokea baaada ya uchaguzi..
Waliyogombea urais ni kina nani?
Kulikuwa na jumla ya wagombea urais 21 lakini wagombea wakuu ni watatu:
- Martin Fayulu, Mkurugenzi mkuu wa zamani wa mafuta ambaye ameahidi nchi yenye mafanikio lakini ambaye watu maskini wanahisi hawezi kuwatetea.
- Emmanuel Ramazani Shadary, Waziri wa zamani wa mambo ya ndani na mtiifu kwa Kabila, ambaye aliwekewa vikwazo na Muungano wa Ulaya kwa hatua zilizochuliwa upinzani wakati wa maandamano ya mwaka 2017.
- Felix Tshisekedi Tshilombo, Mtoto wa mwanasiasa mkongwe ambaye ameahidi kupambana na umaskini.
Zaidi kuhusu DR Congo
Nchi hiyo kubwa ya Afrika ya kati ina utajiri wa madini na ndiyo mzalishaji mkubwa wa madini ya cobalt, yanayotumiwa kwa simu na betri za magari.
Rais Kabila alichukua nafasi ya uongozi baada ya baba yake Laurent Kabila kuuawa mwaka 2001.
Alichaguliwa rasmi mwaka 2006, na baadae akapata tena nafasi ya kuongoza kwa muhula mwingine baada ya uchaguzi mwa mwaka 2011 uliyokumbwa na utata.
Alizuiliwa kugombea tena urais baada ya muhula wake wa mwisho uongozini kukamilika.
Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo rais Kabila alitakiwa kuachia madaraka miaka miwili iliyopita , lakini uchaguzi uliahirishwa baada ya tume ya uchaguzi kusema kuwa inahitaji muda zaidi kuwasajili wapiga kura.
No comments: