Uchaguzi DRC: Wagombea Felix Tshisekedi na Martin Fayulu walalamikia dosari uchaguzi wa urais
Wagombea wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamelalamikia dosari nyingi wanazosema zilitokea wakati wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili.
Milolongo mirefu ya wapiga kura ilishuhudiwa katika vituo vingi na mitambo ikafeli kwenye baadhi ya vituo.
Aidha, upigaji kura uliathiriwa katika baadhi ya maeneo baada ya mvua kubwa kunyesha, huku baadhi ya wapiga kura wakilalamikia majina yao kutokuwepo kwenye sajili katika baadhi ya vituo.
Mmoja wa wagombea wa urais wanaotaka kumrithi Rais Joseph Kabila anayeondoka baada ya kuongoza kwa miaka 17, Felix Tshisekedi, amesema anahofia kwamba huenda hitilafu hizo zilipangwa ndipo kutoa sababu za uchaguzi kufutwa na kumuwezesha Bw Kabila kusalia madarakani.
- EU yalaani balozi wake kufurushwa DRC
- Uchaguzi DRC wazidi kuingia dosari
- Mgombea mkuu wa upinzani DRC Martin Fayulu ni nani?
Wengi wa wapiga kura walitatizika kutokana na hali kwamba mashine zilitumiwa kwa mara ya kwanza kupigia kura.
Aidha, baadhi ya mashine zilifeli.
Bw John Tendwa, ambaye ni jaji mstaafu nchini Tanzania na aliwahi kuhudumu kama Msajili mstaafu wa Vyama vya Siasa nchini humo amesema iliwachukua baadhi ya wapiga kura hadi dakika saba kupiga kura kituoni.
Shughuli ya kuhesabu kura zilizopigwa inaendelea baada ya vituo kufungwa Jumapili jioni na matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa katika kipindi cha wiki moja.
Uchaguzi wa sasa ulifaa kufanyika miaka miwili iliyopita lakini uliahirishwa mara kadha kutokana na kutokamilika kwa maandalizi.
Kabla ya uchaguzi, kulitokea utata baada ya uchaguzi kuahirishwa katika maeneo yaliyoathiriwa na Ebola yakiwemo miji ya Beni na Butembo mashariki mwa nchi hiyo, na pia katika jiji la Yumbi magharibi mwa nchi hiyo.
Hatua hiyo iliathiri takriban wapiga kura 1.26 milioni kati ya jumla ya wapiga kura 40 milioni. Uchaguzi katika maeneo hayo uliahirishwa hadi Machi.
Uamuzi huo ulizua utata ikizingatiwa kwamba rais mpya anafaa kuapishwa kufikia katikati mwa Januari.
Baadhi ya wanaharakati waliandaa uchaguzi wa mwisho uliopewa jina 'uchaguzi wa raia' katika mji wa Goma, mojawapo wa miji iliyoathiriwa, anasema mwandishi wa BBC Gaius Kowene.
Vituo vya kupigia kura vilifungwa saa kumi na moja jioni, lakini watu waliokuwa kwenye foleni waliruhusiwa kupiga kura.
Kabila amesemaje?
Rais Kabila alipiga kura mapema asubuhi mjini Kinshasa katika shule ambayo mgombea anayemuunga mkono, waziri wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Ramazani Shadary alikuwa pia anapiga kura.
Baada ya kupiga kura, aliambia wanahabari: "Ni wazi kwamba uchaguzi huu ni huru na wa haki, na bila shaka utakuwa huru na wa haki."
Alisema wasiwasi wake pekee ulikuwa kwamba mvua ingeathiri idadi ya watu ambao wangejitokeza kupiga kura.
Baraza kuu la maaskofu wa kanisa Katoliki (CENCO) lilisema mashine za kupigia kura zilikumbwa na hitilafu katika takriban vituo 544 kati ya 12,300 katika maeneo ambayo walifuatilia upigaji kura.
Baadhi ya wapiga kura walilalamika kwamba majina yao hayakupatikana kwenye sajili ya wapiga kura.
No comments: